John 17

Isa Ajiombea Mwenyewe

1 aBaada ya Isa kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:

“Baba, saa imewadia. Umtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe.

2

bKwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa.

3

cNao uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe uliye Mungu wa pekee, wa kweli na Isa Al-Masihi uliyemtuma.

4

dNimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye.

5

eHivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujakuwepo.

Isa Awaombea Wanafunzi Wake

6 f“Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako. 7Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako, 8 gkwa kuwa maneno yale ulionipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma. 9 hNinawaombea wao. Mimi siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako. 10 iWote walio wangu ni wako na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao. 11 jMimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 12 kNilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia.

13 l“Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao. 14 mNimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu. 15 nSiombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. 16 oWao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. 17 pUwatakase kwa ile kweli, neno lako ndilo kweli. 18 qKama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo. 19 rKwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.

Isa Awaombea Wote Wamwaminio

20 s“Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao 21 tili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako, wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiye uliyenituma mimi. 22 uUtukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23 vMimi ndani yako na wewe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.

24 w“Baba, shauku yangu ni kwamba, wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani, utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.

25 x“Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma. 26Nimefanya jina lako lijulikane kwao nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili kwamba upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”

Copyright information for SwhKC